MADEREVA 30 WAFUNGIWA LESENI KWA ULEVI DAR

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio mbalimbali yaliyotokea jijini humo.

Na Nora Damian, The Page

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewafungia leseni za udereva madereva 30 kwa makosa ya kuendesha wakiwa wamelewa.

Akizungumza leo Januari 2,2025 na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema madereva hao wamefungiwa leseni kwa miezi sita baada ya kukutwa na kiwango kikubwa cha ulevi ambacho hakikubaliki kisheria kuendesha vyombo vya moto.

"Kabla ya Sikukuu ya Krisimasi tulifanya ufuatiliaji wa tabia za madereva ili kuzuia na kudhibiti vitendo vya ajali za barabarani, tuliwakamata madereva 179 kwa makosa mbalimbali. Madereva 30 tuliwakuta na kiwango kikubwa cha ulevi zaidi ya miligramu 80 ambacho hakikubaliki kisheria.

"Jeshi lilichukua hatua kuwashughulikia waliokutwa na kiwango hicho, waliwekwa mahabusu wasipate furaa ya kuendesha gari, wamefungiwa leseni kwa miezi sita na hatua nyingine zinaendelea," amesema Kamanda Muliro.

Aidha amesema kumekuwa na mafanikio kwa baadhi ya mashauri yaliyopelekwa katika mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam kama vile ulawiti, ubakaji na unyang'anyi wa kutumia silaha ambapo watuhumiwa wamekutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na wengine kifungo cha maisha jela.

Kamanda Muliro amesema wamejipanga kushuka chini na kuwa karibu na wananchi kwa lengo la kupokea taarifa mbalimbali na kuzifanyia kazi huku akisisitiza kuwa hawatakuwa na huruma na mtu yeyote anayejishughulisha na vitendo vya uhalifu.



Powered by Blogger.