KLINIKI YA SHERIA BILA MALIPO YAZINDULIWA KILIMANJARO

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amezindua Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa huo yenye lengo la kutatua changamoto za wananchi katika masuala ya kisheria.

Kliniki hiyo inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Huduma zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe Januari 21 hadi 27, 2025.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kliniki hiyo Babu ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro na kuja kutoa huduma ya kliniki bure kwa wananchi."Tunaishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutoa huduma hii bure kwa wananchi wetu, hii inaonyesha namna ofisi hii ilivyojikita kusogeza huduma kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini," amesema Babu.

Amesema kliniki hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya wanachi dhidi ya Serikali, itawezesha mawakili wa Serikali kusimamia utawala wa sheria na kushirikiana kwa karibu na wadau katika kutatua masuala ya kisheria.

"Ni matumaini yangu itawasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria, kuna timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakuwa inatatua changamoto mbalimbali za wananchi," amesema.

Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kushiriki kwa wingi katika kliniki hiyo ili wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.Awali Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tamari Mndeme, amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi kupitia kliniki hiyo.

"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na tuna wataalamu wa kutosha, tunaamini kupitia kliniki hii changamoto mbalimbali za wananchi zitatatuliwa," amesema Tamari.

Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za kisheria kwa wananchi.



Powered by Blogger.