WAZIRI KOMBO AONGOZA MKUTANO WA DHARURA KAMATI YA MAWAZIRI SADC

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki mkutano wa dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo uliofanyika Desemba 9,2024 umewakutanisha mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Nchi Wanachama za Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa asasi hiyo, Malawi ambayo ni Mwenyekiti ajaye na Zambia ambayo ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake.

Mkutano huo umejikita katika kujadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hususan bajeti ya misheni ya kanda iliyopo nchini humo kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2024 hadi Desemba 2025.Wakati wa mkutano huo Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuchangia misheni hiyo kwa Wizara za Fedha kutoa kipaumbele kwa michango hiyo pamoja na kuonanisha juhudi za kijeshi na kidiplomasia. 

Taarifa ya kikao hicho itawasilishwa katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kitakachofanyika Desemba 11, 2024 na kuongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo kilichotangulia kikao cha mawaziri.



Powered by Blogger.