TCCIA, DUBAI KUSHIRIKIANA KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Chemba ya Biashara Tanzania (TCCIA) imeingia makubaliano na Chemba ya Biashara Dubai kwa lengo la kuimarisha biashara na uwekezaji wa pande hizo mbili.
Takwimu zinaonyesha thamani ya biashara isiyohusisha mafuta kati ya Tanzania na Dubai ilikua kwa asilimia 9 mwaka 2023 na kufikia Dola za Kimarekani bilioni 2.7.
Akizungumza leo Desemba 12,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Biashara lililoandaliwa na Chemba ya Dubai, Rais wa TCCIA, Vincent Minja, amesema sekta zilizopewa kipaumbele ni kilimo, utalii, maendeleo ya miundombinu, nishati, na teknolojia.
"Chemba ya Dubai ni kubwa sana katika Mashariki ya Kati na kwa kusaini makubaliano haya kutawasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kuingia kwenye masoko ya dunia kupitia Dubai.
"Dubai siyo tu kwamba ni kitovu katika Mashariki ya Kati bali dunia nzima. Dunia nzima wananunua vitu kupitia Dubai, kuna baadhi ya vitu hawazalishi mfano 'apple' (tufaa) lakini ni wasafirishaji wakubwa duniani na hakuna shamba la apple Dubai.
"Kwahiyo Watanzania watapata nafasi kubwa ya kufikia kwenye masoko ya dunia kupitia Dubai na ndiyo lengu letu hasa," amesema Minja.
Naye Rais wa Chemba ya Biashara Dubai, Mohammad Ali Rashed Lootah, amesema makubaliano hayo yatafungua njia mpya za ushirikiano wa kimkakati ambao utachangia ukuaji na ustawi wa pande zote.
"Misheni hii inatoa fursa ya kipekee kujenga madaraja ya ushirikiano kati ya jumuiya za kibiashara za Dubai na Tanzania na kufungua njia mpya za ushirikiano wa kimkakati," amesema Lootah.
Aidha amesema hadi kufikia Septemba mwaka huu kampuni 274 kutoka Tanzania zimesajiliwa kama wanachama hai wa Chemba ya Biashara Dubai.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amesema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuvutia uwekezaji ndiyo maana kumekuwa na mikutano mingi kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini.
"Tanzania tuna fursa kubwa, tuna rasilimali za kutosha, tuna maeneo mazuri ya kilimo, sehemu za utalii, madini na nyingine.
"Wenzetu tumewakaribisha na tunafahamu mwaka.2027 tutakuwa na mashindano ya Afcon ambayo yanafanyika hapa Tanzania, kwahiyo tumewakaribisha waje wawekeze kwa sababu tutakuwa na wageni wengi wanakuja kwahiyo tumejipanga kuhakikisha tunawavutia wadau wengi waje kuwekeza," amesema Dk. Jafo.
