SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA

*TCCIA yapongeza mazingira ya ufanyaji biashara nchini


Na Nora Damian, The Page

Serikali imesema itaendeleza jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa lengo la kuboresha shughuli za biashara, uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yamesemwa Desemba 6,2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, wakati akifungua Kongamano la Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi na Mkutano Mkuu wa 49 wa Mwaka 2024 wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Amesema Tanzania na Afrika kwa ujumla inakisiwa kuwa vijana wengi ambao wanaingia katika soko la ajira ambao wanategemea sekta binafsi ndio maana Serikali imeendelea kushirikiana na kutatua changamoto za sekta binafsi.

Ametaja baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kuwa ni pamoja na kufanywa marekebisho ya sheria na kanuni 55 na sheria zingine 16 na kanuni zake zinaendelea kufanyiwa kazi."Serikali imeondoa mwingiliano wa majukumu na kuanzisha mamlaka mfano sasa tuna Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kurahisisha shughuli zenu. Pia imepunguza idadi ya muda wa kupata huduma kutoka siku 14 hadi tatu na kutoka siku saba hadi tatu za kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma,” amesema Dk. Biteko.

Aidha amesema Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA) imepunguza tozo 16 za biashara ambazo kupitia hizo Serikali inapoteza Sh bilioni 37 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi na jitihada za Rais Samia za kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Dk. Biteko pia amezungumzia viashiria vya ukuaji wa uchumi akisema kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme ambapo awali hayakuwahi kuzidi megawati 219 kwa mwaka ambapo kwa mwaka 2024 mahitaji ni megawati 420."Mahitaji ya nishati ya umeme yanaongezeka na hii ni kwa sababu viwanda vingi vimejengwa na uchumi unachangamka. Tunaanza kuona wananchi wanatumia umeme megawati 52 na viwanda vinatumia megawati 48 hii ni kiashiria kuwa uchumi unaendelea kukua vizuri,” amesema.

Amewaasa wafanyabiashara nchini kulipa kodi kwa hiari ili Serikali iweze kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali itakayosaidia utoaji huduma za kijamii kwa wananchi na kuchochea maendeleo huku akiwataka kuzalisha malighafi na bidhaa zenye ubora zitakazovutia masoko na kutoa ajira kwa watu.

Kuhusu mikataba iliyosainiwa ameitaka TCCIA kuwa mawakala wa kutoa elimu ya mlipakodi kwa wananchi ili watu waone heshima ya kulipa kodi.

Amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini huku akivitaka vyama vya kisekta kuepuka migogoro na kusisitiza upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwao.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), John Lukuvi, amesema kongamano hilo la zaidi ya wafanyabiashara na wakulima 300 kutoka nchi nzima ni muhimu kwani kupitia jukwaa hilo Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kukuza sekta binafsi nchini.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mkoa huo umekuwa na ushirikiano mzuri na TCCIA katika shughuli mbalimbali.

Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vicent Minja, amempongeza Rais Samia kwa jitihada za kuifungua nchi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kusaidia biashara kufanyika kwa utulivu.

Amesema taasisi hiyo ina ofisi katika nchi za China, Uturuki na Uingereza hivyo inarahisisha kuunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na nchi mbalimbali.“Tunaishukuru Serikali kwa kurahisisha maendeleo ya biashara katika Bandari ya Dar es Salaam sasa meli zikija na mizigo zinapakua ndani ya siku chache, tunamshuru Rais Samia kwa kuunda tume ya kushughulikia masuala ya kodi,” amesema Minja.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Oscar Kissanga, amesema taasisi hiyo inalenga kuunganisha wadau wa biashara na kukuza sekta ya biashara na kilimo nchini.

“Katika kipindi cha miaka 36 TCCIA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha ushindani na kuvutia wadau wa ndani na nje ya nchi,” amesema Kissanga.

Amesema lengo la TCCIA ni kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi imara huku akimpongeza Rais Samia kwa jitihada za kuhakikisha kunakuwepo na ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi.Kissanga ametaja baadhi ya shughuli za TCCIA katika kipindi cha mwaka 2024 kuwa ni kutoa mafunzo ya kuelimisha Watanzania kuhusu Soko Huru la Afrika kutoka katika mikoa nane, kusafirisha shehena za bidhaa mbalimbali katani ikiwa ni asilimia 70 ya shehena yote.

Vilevile, imefanya ukaguzi wa viwanda 37 na kufanya Jukwaa la Biashara ya Korosho Tanzania na kuleta nchini zaidi ya kampuni 100 pamoja na kuzisaidia kampuni za Tanzania kupata fursa za uwekezaji na masoko kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Trademark Afrika, Elibariki Shammy, amesema taasisi yake inalenga kuisaidia Watanzania na Afrika ili iweze kufanya biashara na dunia na kuwa na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi na kushukuru kwa kuendelea kuaminiwa katika kutekeleza shughuli zao.

Kupitia kongamano hilo Dk. Biteko ameshuhudia utiaji saini wa baadhi ya mkataba ikiwemo mkataba kuwezesha kufanya kazi pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, ushirikiano wa biashara kati ya TCCIA na Chuo Cha Biashara (CBE) ambapo CBE inatarajia kuwa na mitaala ya biashara ya wanagenzi hivyo ushirikiano huo utasaidia kufikia wafanyabiashara watakaosaidia kufundisha wanafunzi.

Mkataba mwingine uliowekwa saini ni wa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wanachama wa TCCIA kulipa kodi kwa hiari kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kurahisisha ulipaji kodi na kutoa elimu ya namna kiwango na muda wa kulipa kodi.

Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu isemayo 'Kuongeza Ufanisi wa Majadiliano na Ushindani wa Mauzo ya Nje kwa Ustawi wa Uchumi'.



Powered by Blogger.