VIFO KARIAKOO VYAFIKIA 13, RAIS SAMIA AAGIZA UKAGUZI MAJENGO YOTE

Na Nora Damian, The Page

Wakati vifo kutokana na jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo vikifikia 13 Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchunguzwa kwa majengo yote yaliyoko katika eneo hilo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Novemba 17,2024 wakati akizungumza na wananchi na kusema hadi kufikia saa 4 asubuhi watu 84 wameokolewa na kufikishwa hospitali na kati yao 26 bado wanaendelea na matibabu.

“Kwa huzuni kubwa tumewapoteza wenzetu 13 katika tukio hilo, Serikali itabeba gharama za matibabu kwa wote waliojeruhiwa na kuhakikisha waliofariki wanasitiriwa ipasavyo.

“Nitoe pole kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na tukio hili, niwaombe Watanzania wote tuwaweke kwenye maombi wote walioathirika na tukio hili na tuwaombee pumziko la amani wenzetu waliotangulia mbele za haki,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema hadi sasa sababu za kitaalam za jengo hilo kuporomoka bado hazijachunguzwa na kwamba kipaumbele kilikuwa kwanza kuwaokoa waliokuwa ndani ya jengo hilo.

“Baada ya zoezi hili kukamilika namtaka Waziri Mkuu aongoze timu ya wakaguzi majengo, waendelee na zoezi la kukagua eneo lote la Kariakoo na tupate taarifa kamili ya hali ya majengo ya Kariakoo ilivyo. Jeshi la Polisi lipate taarifa kamili kwa mmiliki wa jengo lililoporomoka jinsi ujenzi ulivyokuwa umefanyika…taarifa za uchunguzi zitawekwa wazi na hatua zitakazochukuliwa na Serikali zitaelezwa kwa kina,” amesema Rais Samia.






 


Powered by Blogger.