CUF WALIA WAGOMBEA WAO KUENGULIWA UCHAGUZI WA MITAA

Na Nora Damian, The Page

Chama cha Wananchi (CUF) kimewataka viongozi wake katika maeneo mbalimbali nchini kuwaongoza wagombea walioenguliwa kuandika barua kwa wasimamizi wasaidizi kupinga kutoteuliwa kugombea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa habari Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, amesema baadhi ya wagombea wao katika maeneo mbalimbali nchini wameenguliwa kwenye zoezi la uteuzi lililofanyika jana. 

Ameyataja maeneo ambako baadhi ya wagombea wao wameenguliwa kuwa ni Halmashauri ya Misungwi, Ubungo, Wilaya ya Mtwara Vijijini, Wilaya ya Magu, Wilaya ya Kondoa Mji, Wilaya ya Kondoa Vijijini, Wilaya ya Bukoba Vijijini, Wilaya ya Handeni, Wilaya ya Geita, Wilaya ya Tunduru, Wilaya ya Kinondoni na Wilaya ya Mtwara Mjini.

“Wagombea wetu wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi wameenguliwa kwa sababu ambazo zipo nje ya kanuni zinazosimamia uchaguzi huu, wasimamizi wasaidizi na wasimamizi wa uchaguzi hawakuwa wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na wagombea wetu na kushindwa kuelewa hasa ni siku ipi ya uteuzi.

“Wilaya ya Mtwara Vijijini ambako tuliweka wagombea karibu vijiji na vitongoji vyote, wagombea wetu karibu wote wameenguliwa kwa sababu tofauti ambazo wamezieleza wasimamizi. Hali hii inatia shaka na kukatisha tamaa katika juhudi zetu za ujenzi wa demokrasia na ujenzi wa taifa lenye viongozi wanaotokana na maamuzi ya wananchi,” amesema Sakaya.

Ameziomba mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo kuzingatia na kufanyia kazi haraka malalamiko yao kuanzia zoezi la uandikishaji, uchukuaji wa fomu na uteuzi wa wagombea.

“Tunamtaka Waziri wa Tamisemi kutoa maagizo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi kuwarejesha wagombea wetu wote. Pia tunamuomba mheshimiwa Rais kuingilia kati mchakato huu ili kuondoa sintofahamu zinazoendelea,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema siku chache zilizobaki zinatosha kuondoa kasoro hizo na kuruhusu wananchi, vyama vya siasa na wagombea washiriki kwenye uchaguzi kwa amani na utulivu na kuwapa fursa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

Chama hicho kimewaomba wananchi na wanachama wake kuwa watulivu wakati wakisubiri mamlaka husika kuchukua hatua zinazostahili.


 


 

Powered by Blogger.