WAZIRI LUKUVI AVIHAKIKISHIA VYAMA MAAMUZI YA WANANCHI YATAHESHIMIWA UCHAGUZI WA MITAA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, akizungumza wakati alipotembelea Chama cha Wananchi (CUF), Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema maamuzi yatakayofanywa na wananchi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yataheshimiwa na kwamba yaliyotokea mwaka 2019 hayatajirudia. 

Lukuvi ametoa hakikisho hilo leo Oktoba 8,2024 wakati alipotembelea vyama vya siasa vya United Democratic (UDP), NCCR – Mageuzi, National League for Democracy (NLD) na Chama cha Wananchi (CUF).

Amesema dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha falsafa yake ya 4R na ameelekeza watendaji wote wa serikali washirikiane kuhakikisha kanuni zilizowekwa zinaheshimiwa na kusimamiwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan, akizungumza wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi (Wapili kushoto), alipotembelea chama hicho.

“Hamasisheni wanachama wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kugombea, kila mshiriki wa uchaguzi asimamie kanuni ili uchaguzi uwe wa heshima, huru na haki…maamuzi ya wananchi yataheshimiwa ndiyo dhamira ya mheshimiwa rais,” amesema Lukuvi.

Aidha amesema hakuna maeneo ya utawala kama vile kijiji au mtaa yaliyoongezwa na kwamba vijiji vilivyokuwa vimefutwa vimerejeshwa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi, Joseph Selasini, amesema watashiriki uchaguzi lakini akashauri utengenezwe utaratibu utakaosaidia vyama visivyokuwa na ruzuku kuweza kushiriki na kuwa na ushindani ulio sawa. “Ushindani ni mkubwa hatuna ruzuku, hatuna njia yoyote ya kuweza kusaidia uchaguzi zaidi ya wanachama wenyewe, kama kweli tunataka demokrasia katika nchi hii suala la kugharamia demokrasia ni kubwa zaidi. 

“Wengine wanafanya kampeni kwa miguu, wengine wanatumia baiskeli, pikipiki, magari, ndege huko tunajidanganya, utengenezwe utaratibu utakaosaidia vyama,” amesema Selasini. 

Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan, ameshauri kanuni zitolewe mapema ili vyama viweze kuzifahamu na kujiandaa na uchaguzi huo. 

“Chama chetu hakina sera ya kususa uchaguzi kwa sababu uchaguzi ndiyo njia pekee ya kupata uongozi wa nchi, tunaomba uchaguzi huu uwe kielelezo cha kukua kwa demokrasia nchini…yasitokee yale ya 2019,” amesema Doyo. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema suala la wagombea kudhaminiwa na ngazi ya chini ya chama linaweza kusababisha wagombea wengi kuenguliwa na kuomba liangaliwe upya. 

“Orodha ya vijiji na mitaa haipo hata Tamisemi, tutashindwa kuwapa miongozo viongozi wetu wa chini, tunahitaji kujenga siasa za wazi na za kistaarabu,” amesema Profesa Lipumba. 


Powered by Blogger.