TADB YAWEKA DHAMANA YA SH BILIONI 30 ZA WAKULIMA EXIM BENKI

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege (kushoto) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fedha Benki ya Exim, Shan Kinswaga (kulia), wakisaini mkataba wa makubaliano ya kukopesha wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS).

Na Nora Damian, The Page

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imezidi kuongeza taasisi za kuwakopesha wakulima baada ya kuingia makubaliano ya miaka mitano na Benki ya Exim kutoa dhamana ya mikopo ya Sh bilioni 30 kwa sekta ya kilimo ikijumuisha ufugaji na uvuvi.

Exim inakuwa taasisi ya 17 kuingia makubaliano ya kukopesha wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS).

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank
Nyabundege, alisema lengo ni kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima ambapo watatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hasa kwa vijana, wanawake na miradi inayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema hadi kufikia Aprili 2024 mikopo iliyodhaminiwa na TADB kupitia mfuko wa SCGS imefikia Sh bilioni 300, wanufaika wa moja kwa moja wakiwa 23,940 na wasio wa moja kwa moja ni 897,900 kwa mikoa 27 ya Tanzania Bara na visiwani.

“Benki ya TADB inatambua changamoto ya upatikanaji wa mikopo nafuu inayowakabili wakulima nchini ndiyo maana inaongeza nguvu na ushirikiano wa mabenki na taasisi za fedha ili kutoa mikopo kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema Nyabundege.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga, alisema anaamini ushirikiano huo utakuwa na tija kiuchumi na maendeleo kwa wajasiriamali wadogo ambao walikuwa wakikosa mikopo kwa sababu ya vigezo.

Alisema mikopo hiyo itasaidia Watanzania kuingia kwenye kilimo biashara badala ya kufanya kilimo cha kujikimu pekee.

“Exim benki tunaamini katika usawa ushirikishwaji wa kifedha kwa makundi yote bila ubaguzi, tunajua wengi walikuwa wakikwama kupata mikopo katika kuendeleza shughuli zao lakini kupitia ushirikiano huu tutawafikia wengi,” alisema Kinswaga.
Powered by Blogger.