WASICHANA MILIONI 4.8 KUCHANJWA SARATANI YA KIZAZI TANZANIA


Na Nora Damian, The Page


Zaidi ya wasichana milioni 4.8 wenye umri wa miaka 9 hadi 14 walioko shuleni na nyumbani wanatarajiwa kupatiwa chanjo kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi ambayo sasa itatolewa dozi moja badala ya mbili kama ilivyokuwa awali.

Tafiti zinaonyesha saratani ya mlango wa kizazi inaweza kudhibitiwa kwa wasichana kabla hawajapata maambukizi kwa kupatiwa dozi moja ya chanjo kabla hawajaanza vitendo vya kujamiiana vinavyoweza kusababisha maambukizi.

Akizungumza Aprili 20,2024 wakati wa mkutano kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi Mkurugenzi wa Kinga, Dk. Ntuli Kapologwe, amesema chanjo hiyo ni salama imethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Kamati ya Kitaalam ya masuala ya Masuala ya Chanjo.

Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe, akizungumza wakati wa mkutano kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika lisilo la kiserikali TIP linaloundwa na taasisi nne za kidini ambazo ni Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar (MoZ).

“Serikali imechukua jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa inawalinda wasichana kwa kuwapatia chanjo ya kudumu wakiwa katika umri mdogo, sote tuna wajibu wa kuhakikisha walengwa wote ambao hawajapata chanjo wanapata kulingana na ratiba,” amesema Dk. Kapologwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la TIP, Asina Shenduli, amesema watashirikiana na Serikali kuhakikisha elimu juu ya chanjo hiyo inatolewa na viongozi wa dini kupitia fursa mbalimbali ikiwemo nyumba za ibada.

“Sote tunatambua umuhimu wa viongozi wa dini, wana sauti na sauti zao zinasikika, zinaaminika na kuheshimika hivyo, tushirikiane na Serikali na Unicef kuhakikisha elimu inatolewa,” amesema Shenduli.

Naibu Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Chesco Msaga, akizungumza wakati wa mkutano kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.

Viongozi wa dini walioshiriki mkutano huo wamewahamasisha wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika chanjo hiyo ili waweze kukingwa dhidi ya ugonjwa huo.

Naibu Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Chesco Msaga, amesema watoto wakiweza kuokolewa na kuepushwa na saratani hiyo jamii kubwa itaokolewa.

Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar, amesema elimu ya chanjo hiyo ikitolewa nchini kuhusu chanjo hiyo watapatikana watu wenye afya bora watakaosaidia kuleta maendeleo ya nchi.

Takwimu zinaonyesha saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kuliko saratani zingine nchini ambapo utafiti wa NIMR wa 2019/20 hadi 2021/22 ulionyesha watu 17,757 waliugua saratani na kati yao asilimia 22.5 walikuwa na saratani ya mlango wa kizazi huku mikoa iliyoongoza ikiwa ni Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza.







Powered by Blogger.