RUKSA MAGAZETI KUSOMWA KWA MBWEMBWE
Na Nora Damian, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameondoa zuio lililokuwa limetangazwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) la kuzuia waandishi wa habari kusoma magazeti kwa ubunifu.
Februari 14,2024 TCRA kupitia kwa Meneja wa Huduma za Utangazaji, Andrew Kisaka, ilisema itawachukulia hatua watangazaji wanaosoma magazeti kwa mbwembwe huku wakiongeza baadhi ya vitu wakati wa usomaji.
Leo Februari 15,2024 kupitia katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Waziri Nape amekosoa zuio hilo la TCRA na kuitaka ijenge utamaduni wa kuzungumza kabla ya kuagiza.
"Nimeuona mjadala wa kusoma magazeti nimeelekeza TCRA kuruhusu ubunifu kwenye tasnia ya habari, staili ya usomaji wa magazeti imeongeza mvuto kwenye usomaji huo, ni jambo ambalo linapaswa kutiwa moyo badala ya kuzuiwa," amesema Nape.
