RAIS SAMIA; MIAKA 47 YA CCM IMEKUWA NA MAPINDUZI MAKUBWA

Rais Samia Suluhu Hassan.

Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wakati chama hicho kikiadhimisha miaka 47 toka kuanzishwa kwake wanajivunia kimepiga hatua kubwa za kujivunia.

Katika ukurasa wake wa X Rais Samia ameandika akiwatakia heri ya miaka 47 toka kuanzishwa kwa chama hicho.

"Imekuwa miaka 47 ya mapinduzi makubwa kwa kila Mtanzania kwenye kila kona ya nchi yetu. Tulipo leo, sipo tulipokuwa miaka 47 iliyopita.

"Tumepiga hatua kubwa za kimapinduzi na za kujivunia zenye matunda mazuri katika uchumi wetu, miundombinu yetu, huduma zetu za afya, maji, kilimo, elimu, nishati, utawala bora, uhuru wa watu, haki na maendeleo kwa ujumla. Katika miaka hii 47 tumeendelea pia kubaki wamoja, wenye amani na mshikamano, tunu ambazo hazijawa rahisi kupatikana, kutunzwa na kudumu katika maeneo mengi ya bara letu.

"Maendeleo ni mchakato, ni hatua inayotaka juhudi na weledi wa kila mmoja wetu. Tafakuri na sherehe za miaka 47 ya kuzaliwa kwa chama hiki muhimu kwa historia, umoja, uimara na maendeleo ya nchi yetu ziendelee kutusukuma mbele kuifanya vyema kazi iliyo mbele yetu; kazi ya kuhakikisha tunaipatia majawabu kila changamoto inayomkumba Mtanzania popote pale alipo kwa kiwango cha juu kabisa. Kidumu Chama Cha Mapinduzi," ameandika Rais Samia.
Powered by Blogger.