KISARAWE WAMUOMBA RAIS SAMIA AWASADIE WALIPWE FIDIA


Na Mwandishi Wetu, Pwani


Wakazi wa eneo la Bomani katika Mji mdogo wa Kisarawe wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kulipwa fedha za fidia ya makazi yao ili waweze kupisha eneo hilo.

Wakazi hao wanatakiwa kupisha eneo hilo la Jeshi Kikosi cha 191 wilayani humo mkoani Pwani.

Wakizungumza na waandishi wa habari Februari 21,2024 wakazi hao 31 wa eneo la Bomani maarufu ‘barabara ya jeshi’ wamesema licha ya kukubali kuhama kupisha eneo hilo kama walivyotakiwa na mamlaka za Serikali lakini mpaka sasa hawajalipwa fidia zao.


Kiongozi wa wananchi hao, Robert Nyampiga, amesema waliuziwa nyumba hizo zilizopo hatua chache kutoka ilipo Kambi ya Jeshi Kikosi cha 191 na Serikali kupitia Wakala wa Nyumba mwaka 2005.

Amesema tathmini ya nyumba na makazi yao ilikwishafanyika na wamefuatilia hadi hazina lakini hawajapata muafaka wa lini wataingiziwa malipo yao ya fidia ili waondoke kwenye eneo hilo.

“Nyumba hizi wengi tulionunua ni wastaafu kutoka sekta mbalimbali, na baadhi yetu tulikwishafungua biashara ndogondogo ili kujikimu, lakini walipotutaka kuhama walituambia tusiendeleze kitu chochote labda tulime mchicha tu kwani tungelipwa ndani ya miezi minne.

“Mpaka sasa yapata mwaka sasa hatuoni chochote, hatuambiwi chochote tumebaki na sintofahamu” amesema Nyampiga.

Mwananchi maingine Geofrey Mdoe amesema hali imekuwa ngumu kwao baada ya nyumba zao kuanza kuvuja na kuharibika.


“Tunazidi kuwa na wasiwasi kwamba hili eneo bado linatakiwa na wahusika, tunashangaa tangu tumefanyiwa tathmnini ni mwaka mmoja sasa, sasa kama hili eneo hawalitaki tena wafute tathmini yao ya awali ili sisi tuendelee kufanya maendeleo katika nyumba zetu.

“Ndugu mwandishi angalia hili ni duka langu (anamwonyesha mwandishi paa la duka lake), nimelifunga kwa sababu linavuja lote na siwezi kubadilisha hata bati, kimsingi tumefungwa mikono na miguu, tunahitaji kauli na vitendo kutoka kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan," amesema Mdoe.

Mhanga mwingine, Maliselina Macha amesema kinachomuumiza alifunga biashara zake baada ya kuambiwa wanatakiwa kuhama ndani ya miezi minne.

Amesema alikuwa na duka la vinywaji ambavyo alivinunua kupitia mkopo wa halmashauri na kulazimika kuviuza kwa hasara akitarajia kuhama katika eneo hilo.

“Niliamua kuuza bidhaa zote za dukani pamoja na mifugo yangu ili kupisha makazi haya ambayo tuliambiwa nikwa ajili ya usalama. Hatuna pingamizi na hilo isipokuwa jambo hili limetusababishia msongo wa mawazo, nyumba zetu zimebomoka, hatuna mahali hata pa kujisaidia, tunateseka hatima yetu hatuijui, tumaini letu pekee ni kwa mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa hizi atuone na kutusaidia” amesema Maliselina.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatuma Almasi Nyangasa, hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya Katibu mukhtasi wake kusema alikuwa kikaoni.

Kwa upande wake, Kamishna wa majengo na maeneo yote ya jeshi, Kanali Yenu Maguguli alipoulizwa amesema wenye mamlaka ya kufanya malipo hayo ni hazina, hivyo aliwataka wananchi kuvuta subira kwani anaamini haki itatendeka.
Powered by Blogger.