KILICHOMUUA EDWARD LOWASSA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Na Nora Damian

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amefariki dunia huku sababu za kifo chake zikitajwa kuwa ni baada ya kuugua magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

Kifo cha Lowassa kimetangazwa Februari 10,2024 na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Amesema Lowassa amefariki Februari 10,2024 saa nane mchana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Amesema Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu Januari 14,2022 hospitalini hapo na baadaye alipelekwa kwa matibabu zaidi nchini Afrika Kusini ambapo alirejea tena JKCI alikopatwa na mauti.

“Kutokana na kifo hicho Rais Samia ametangaza siku tano za maombelezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia Februari 10,2024. Taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitaendelea kutolewa na Serikali," amesema Dk. Mpango.

Lowassa alizaliwa Agosti 26,1953 katika Kijiji cha Ngarash Monduli na katika familia ya mzee Ngoyai Lowassa yeye ndiye alikuwa mtoto mkubwa wa kiume.

Powered by Blogger.