BARABARA YA HARAKA KIBAHA – CHALINZE MBIONI KUANZA

Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila, akizungumza wakati wa kufungua zabuni kwa wawekezaji walioomba kujenga barabara ya Kibaha - Chalinze. Kulia ni Meneja wa Miradi ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Mhandisi Kitainda Michael.


Na Nora Damian, Dar es Salaam

Utekelezaji wa mradi wa barabara ya mwendokasi Kibaha - Chalinze kilomita 78.9 uko mbioni kuanza baada ya kukamilika kwa zoezi la kuchambua zabuni kwa waliokidhi vigezo vya kuijenga.

Serikali inakusudia kujenga barabara ya kulipia Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro kilomita 250 kwa utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ambapo awamu ya kwanza itahusisha kilomita 78.9.

Akizungumza leo Februari 6,2024 wakati wa kufungua zabuni kwa wawekezaji walioomba kujenga barabara hiyo, Meneja wa Miradi ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Mhandisi Kitainda Michael, amesema awamu ya kwanza ya Kibaha hadi Chalinze itatekelezwa kwa miaka mitatu.

“Kampuni tisa ziliwasilisha nyaraka zao za zabuni na baadaye kamati ilipendekeza kampuni tano, kisha baada ya uchambuzi zilipatikana tatu. Tunaendelea kufanya tathmini ili tuweze kumpata mwekezaji mzuri atakayepewa jukumu la kutekeleza mradi huu wa sehemu ya kwanza ya Kibaha hadi Chalinze,” amesema Mhandisi Michael.

Naye Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila, amesema mradi huo ukikamilika utapunguza muda wa kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro hivyo kukuza uchumi kwani watu watafika sehemu wanazokwenda kwa wakati.

“Mradi utaongeza fursa mpya za ajira kwa jamii, utawezesha upatikanaji wa ujuzi, ufundi, fedha, teknolojia na kimenejimenti kutoka sekta binafsi. Utahamisha vihatarishi vya mradi kwa kiwango kikubwa kwenda kwa sekta binafsi kwani mwekezaji ndiye atakayebeba vihatarishi vyote kuanzia usanifu, ujenzi na uendeshaji,” amesema Kafulila.

Aidha amesema mradi huo utawezesha upatikanaji wa mtaji wa uwekezaji hivyo kupunguza deni la taifa na utegemezi kutoka kwa wafadhili.

Kafulila amesema pia mradi huo utapunguza mzigo wa kibajeti kwa Serikali katika kutekeleza mradi huo na kuimarisha uwezo wa Serikali kutoka huduma za kijamii kwa ufanisi.

Kulingana na Tanroads kazi ya upembuzi yakinifu inaendelea kwa sehemu ya pili ya mradi huo kilomita 126.1 (Chalinze – Morogoro).

















Powered by Blogger.