KASEKENYA AIAGIZA TANROADS KUJA NA MIPANGO YA MUDA MREFU UJENZI WA MADARAJA
Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya (katikati), akiangalia Barabara ya Kunduchi – Mbuyuni – Ununio iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam.
Serikali imeagiza Wakala wa Barabara (Tanroads) kuja na mipango ya muda mrefu ya kutengenezea njia sahihi maji ili yasiwe chanzo cha kubomoa madaraja.
Akizungumza Januari 22,2024 wakati wa kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua katika Jiji la Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha mafuriko, kukatika kwa barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Tanrodas muhakikishe mnakuja na mipango ya muda mrefu kuangalia miundombinu ya madaraja yaliyopo na kama haitoshelezi yajengwe kwa kuwekwa kingo sahihi ili maji yasiathiri miundombinu hiyo.
“Wananchi pia tuhakikishe hatufanyi shughuli za kibinadamu kwenye mito, hatujengi kwenye mikondo ya maji, kama shughuli kibinadamu zitaendelea kufanyika watu wakatupa taka ngumu, wakafanya kazi karibu na mapito ya maji changamoto hii hatutaepukana nayo,” amesema Kasekenya.
Kasekenya ambaye alikagua Barabara ya Kunduchi – Mbuyuni – Ununio iliyokatika baada ya maji kubadili uelekeo na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano, aliridhishwa na kazi iliyofanyika na kuiagiza Tanrodas kuhakikisha wanafungua upande wa pili wa barabara hiyo.
Kuhusu Daraja la Jangwani amesema kuna mpango mkubwa wa kulijenga lakini litaendelea kufunguliwa kila linapoziba ili liendelee kupitika.
Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Suzana Lucas, amesema athari kubwa zilizotokana na mvua hizo katika jiji hilo ni kuharibika kwa miundombinu ya barabara na madaraja.
“Tumekuwa tukifanya kazi kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa tangu lilipotokea tatizo na tuliahidi kwamba ndani ya saa 48 tutahakikisha tunaifungua barabara hii… tumefanya kazi usiku na mchana na tumefanikiwa kufungua,” amesema Lucas.
Amesema sehemu iliyokuwa na uwazi walifanikiwa kujaza mawe na kuweka zege na kuyaelekeza maji yarudi kwenye mkondo wake na kutoa takataka zilizokuwa zilemetwa na mvua na kuziba midomo ya daraja.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema wamesafisha mito na mitaro ya maji ya mvua na kutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari hasa wanapopita kwenye barabara zilizojaa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada walizochukua kukabiliana na athari za mvua.
“Tuliwaambia wananchi tuna maafa lakini si maafa makubwa ya kuishinda Serikali, Tanroads na Tarura wamefanya kazi kubwa kuanzia daraja la Mpiji tulikesha nao na hili la Kunduchi Mtongani kuhakikisha huduma ya usafiri inarejea,” amesema Mtambule.



